‘Kipande Cha Keki’ ni usemi uliofasiriwa moja kwa moja (kimakosa) toka Lugha ya Kiingereza. Ina maana ya kuashiria wepesi wa kutekeleza jambo. Tafsiri hii ya Kiswahili ilitumika hivi majuzi katika ujumbe iliyodhaminiwa na kampuni ya Subway nchini Marekani. Ujumbe huu ulihusisha Wakenya halisi watatu waliokuwa wakiigiza Wana-Riadha wa masafa marefu. Wakenya Marekani kote walifurahia kutambulika kwa Kenya kupitia udhamini huu. Bila shaka, Wana-riadha Wakenya wanastahiki pongezi kwa majivuno na sifa waliotunuku nchi ya Kenya na Bara la Afrika. Wana-riadha hawa ni mashujaa waliomakininika na nidhamu na kujitolea kwao unasifika kimataifa. Kupitia udhamini huu na furaha iliyofuata, Kenya ilijitosa katika fedheha kwa jambo tunalochukulia kwa turathi la kitaifa. Ni jambo la kusitikisha kwamba hadi kufikia uandishi wa nakala hii, wengi miongoni mwa Wakenya bado hawatambui ni Fedheha ipi udhamini huu uliyozua.
Siku iliyofuata kupeperushwa kwa udhamini huu, nilipokea simu toka rafiki yangu Mzungu aliyejifunza lugha ya Kiswahili kupitia Taasisi ya Kiswahili Kisiwani Unguja .Kawaida yake hunipigia simu kwa nia ya kuboresha umahiri wake katika lugha. Si jambo la kushangaza aliponiuliza maoni yangu kuhusu ujumbe huo wa Subway kwani si kawaida kupata ujumbe wa Kiswahili katika vituo vya Marekani. Kwa ufasaha na lafdhi ya Kiuguja, aliniuliza “Ndugu yangu, Kwanini katika ujumbe huu uliodhaminiwa na Subway, Waswahili hawa wanazungumzia Keki ilhali kijihoteli cha Subway hawana mapishi ya keki wala vitu vya sukari?” Hatutoingilia kwa undani mazungumzo ilyofuatia. Swali lake lilishurutishwa na ujuzi aliyopata kisiwani Unguja wa kuweza kuyaziba mafikra katika lugha nyingine anapozungumza Kiswahili. Uzoefu huu una umuhimu wa kuimarisha mtiririko wa lugha na ufasaha kwa ujumla. Haikuwa bayana kwake kwamba kulikuwa na ufasiri wa kimakosa na kisha nikamfafanulia.
Usemi huu wa ‘Kipande cha keki’ ulifasiriwa neno kwa neno kutoka Kiingereza, hivi basi kuyazamisha mawazo yaliyotarajiwa na mhariri wa ujumbe huu. Wengi miongoni mwa wa Kenya waliitizamia kama mzaha au kejeli. Ukweli mtupu ni kwamba ilikuwa ni kosa kubwa katika matumizi ya lugha ambayo haikubainika. Hali duni kwa Lugha ya Kitaifa ya Kiswahili katika Jamuhuri ya Kenya ilifuchuliwa na kufukuliwa na ujumbe huu. Kwa kweli, siwezi kudai kwamba nina ujuzi wa utafiti na matayarisho yanayozingatiwa hasa kwa Ujumbe wa lugha za kigeni hapa Marekani. Lililo bayana ni kwamba, mamia ya maelfu au mamilioni za dola hutumika katika matayarisho ya ujumbe hizi kwasababu ya makadirio ya mapato maridhawa. Ujumbe huu ulihusisha washirika watatu Wakenya na kuna uwezekano walipata usaidizi toka kwa kundi la wafasiri ingawa hatukupata mbinu ya kuthibitisha. Mbali na hayo, ujumbe huu ulipeperushwa kwa watazamaji wengi sana wa kimataifa. Wakenya walizidi kuifurahia na kushangilia pasina kufahamu makosa yaliyohusishwa. Sehemu hiyo ya ‘Kipande cha Keki,’ ilichanjwa kisiri kutoka ujumbe huo wiki chahche baadaye, hivi basi kuleta afueni kidogo kwamba wahariri walikosolewa.
Kosa katika tangazo hili la ‘Subway’ si kosa kubwa la kipekee kuwahi kutukia katika Lugha ya Kiswahili. Tuliangazia kosa hili kwa kuwa ilifanyika katika kiwango cha kimataifa mbeli ya Umati mkubwa wa watu miongoni mwao wakiwa wazungumzaji wa Kiswahili wasio Wakenya. Kuna kisa maarufu inayosimulia misafara na misukosuko ya Lugha ya Kiswahili. “Kiswahili kilizaliwa katika Kisiwa cha Unguja, ikastawi na kuimarika Tanzania Bara, ikakumbwa na maradhi hatari ilipopitia Kenya na mwishowe kufariki ilipowasili Uganda. Waganda wakalitia kwa Jeneza na kulisafirisha hadi Congo kwa mazishi na mazingaombwe yake yameanza kujitokeza nchini Rwanda na Burundi.” Ikiwa Lugha ya Kiswahili kitakuja kupotea, Lawama bila shaka itakuwemo mikononi mwa Wakenya. Katika visa hivi vya Misafara maarufu ya Lugha ya Kiswahili, Kenya ndio ilikuwa sehemu ya mwanzo ya Lugha kupata misukosuko mifano ya magonjwa ya kuambukiza inayozidi kuenea na kuleta gharika. Wakenya walipokea motto mwenye afya na bashasha kutoka ndugu zetu watanzania, Lakini tukawakbidhi Waganda motto mwenye maradhi wakajaribu kumtibu lakini akafariki akiwa bado barobaro. Wenzetu kutoka Congo waliokuwa wakisubiri Kiswahili kwa hamu na ghamu, walipokea mzoga toka kwa kwa Waganda na wakaamua kumzika kaika Pori za Bukavu ambapo hadi leo kuna Waswahili mle. Wanyarwanda na Warundi waliokadiria kulea Kiswahili hadi makamo, walihuzunika waliposimuliwa Visa na Mikasa ilyokumba Kiswahili katika misafara yake. Hivi basi waliamua kuyazindua mazingaombwe yako na Kiswahili bado yatumika sehemu hizo.
Sisi Wakenya, tumejimudu kuivunja Lugha yetu ya kitaifa. Dhidi ya hayo, kuna mikakati na hatua ambazo tumechukua kujaribu kuleta tiba kwa madhara iliyoathiri Lugha ya Kiswahili. Rais wa kwanza wa Jamuhuri ya Kenya, Hayati mzee Jomo Kenyatta aliiwezesha Kiswahili kukubalika kama lugha ya taifa, kufuatilia mwelekeo wa Tanzania. Katika miaka ya sitini, nchi za Afrika zilikuwa katika hali ya kujikakamua kujitambulisha. Kukubalika kwa Lugha ya Kiswahili ilikuwa ni fanikio kubwa sana na tunawashukuru wote walioiwezesha . Mfumo wa 8-4-4 wa elimu nchini Kenya ulibuniwa chini ya utawala wa Daniel Arap Moi. Mfumo huu ulikuwa na manufaa na madhara yake lakini la muhimu ni Kwamba Kiswahili kilifanywa somo la lazima na kutahiniwa katika mitihani ya Kitaifa. Hatua hii iliokoa lugha Kiswahili na ikawa chanzo cha umoja nchini Kenya wakati ambapo watu fulani walijaribu kuipiga vita. Mbali na mikakati ya kiserikali, mwendo wa mwaka wa 2000 au hapo karibuni, vyombo vya habari vya kibinafsi nchini Kenya ilianza kupeperusha matangazo kwa Kiswahili. Bila ya kusahau Magazeti kama Taifa Leo na Kenya leo ambazo tayari zilikuwa zikichapishwa. Kuanza kwa utangazaji wa Lugha ya Kiswahili kupitia NTV, KTN na karibuni zaidi Citizen na K24, kulileta mabadiliko na kufanya Kiswahili Fasaha kukubalika na kizazi kipya kama njia ya mawasiliano. KBC ilikuwa kituo cha pekee hapo awali ilipokuwa maarufu kwa kueneza propaganda na watu hawakuwatilia maanani sana lakini wanastahiki kutajwa kwa mchango wao wa lugha ya Kiswahili. Citizen TV wanastahiki kutajwa kwa mkazo zaidi kwani wamezipa vipindi vya Kiswahili kipo umbele ukiwalinginisha na vituo vingine. Kuna wengine wengi miongoni mwetu waliochangia kuendeleza Kiswahili nchini Kenya kama walimu na wasomi. Hatuna uwezo wa kuwataja wote katika nakala hii.
Swali muhimu kwa sasa ni Je, tumefanya vya kutosha kuimarisha Lugha hii ambayo tuliivunja? Kwa kweli, hatujakaribia kamwe lakini tuna msingi bora kufuatia mikakati niliyotaja hapo awali. Hakuna mwelekeo Fulani maalum itakayoimarisha Kiswahili kwa Haraka lakini mna maoni tofauti. Kuna mitazamo mbali mbali kutoka kwa Wasomi wa Kiswahili, Walimu, Wana Harakati wa elimu, Waandishi wa vitabu, wana-siasa, wazazi na washirika dau wengine. Baadhi ya Wasomi wanapendekeza tufuate mfumo ya kufunza masomo yote kwa Kiswahili. Kundi lengine la Wasomi lainapendekeza kujumuisha mafunzo ya maandishi pamoja na mafunzo ya uzungumzi kuimarisha ujuzi wa kuzungumza. Waandishi, wanapendekeza kuleta destruri ya usomaji wa vitabu kutoka chekechea hadi shule ya upili. Wana-siasa wanatofautiana kwa maoni kulingana na eneo bunge lao na posho wanalotarajia. Wazazi wana nia ya kuona matokeo bora pasina kujali zaidi mapendekezo itakayotekelezwa. Wana Harakati wa elimu wamenaswa kadamnasi ya wingi wa maoni haya na wanatofutiana wenyewe kwa wenyewe. Wataalamu wote hawa wana maoni mazuri. Kuna umuhimu wa kuyaorodhesha kwa njia ya uadilifu na busara kuhakisha kwamba viwango vya Kiswahili vitaimarika bila ya kupunguza au kuyapuuza masomo mengine katika mfumo wetu wa elimu.
Hatua ya kwanza inayoweza kutekelezwa kwa urahisi ni kuwajibika kwa walimu wa Kiswahili katika kubadili mtindo na mwelekeo wa kufunza lugha. Ukilinganisha na Sayansi, Mafunzo ya Lugha ina wepesi kwani mwalimu ana uhuru wa kuchagua mada ya kuchambua darasani kimasomo. Walimu wa Kiswahili wanapasa kutumia ubunifu wao katika kuchagua mada watakazojadili darasani kuimarisha lugha na kusisitiza michango kutoka kwa wanafunzi. Katika darasa la kidato cha kwanza kwa mfano, ambapo wengi wa wanafunzi ni kati ya miaka kumi na minne au mitano. Badala ya kuchambua kisa cha Mwalimu Jini au Bwana Tumbo mwenye Shamba, mwalimu angejaribu kuangazia na wanafunzi washindi wa Chaguo la Teeniez na kuwajadili darasani. Waulize kuhusu Wasanii wanaowapenda na watoe maoni ni kwa nini wanaipenda miziki yao. Wanafunzi watakuwa na ari kuyajadili mambo wanayoyapenda. Mwalimu atatumia majadiliano haya kuwaelekeza wanafunzi kwa matumizi ya lugha, semi na msamiati. Vijana waliobalehe hawafurahii kujadili visa vya Mwalimu Jini na utawapata wakisinzia darasani. Ukiwa mwalimu katika shule ya wasichana, jadili mashairi ya Msanii Ali Kiba ya Mac Muga au Cinderella. Waulize wasichana wayalinganishe mashairi haya na yale ya Jaguar kama Kigeugeu au Nimetoka Mbali. Utastaajabishwa jinsi wanawali hawa watakufungulia roho kwa mapenzi yao ya Muziki. Vile vile, mwalimu atanufaika kwa kutumia fursa hii kuwaongoza katika matumizi ya lugha. Wana-dada hawa hawamjali BwanaTumbo Mwenye Shamba. Wataanza kuandika vijibarua kwa marafika zao wa kiume mwalimu akipoteza wakati mbele ya Darasa akieleza kuhusu vile Bwana Tumbo mwenye shamba alipanda viazi na kuchimba kisha akapata almasi. Wazo hili kwa sasa laonekana kama hadithi ya paukwa pakawa. Mtindo huu lakini utawawezesha wanafunzi kuimarisha ufasaha wao na ujuzi wao katika matumizi ya Lugha na msamiati. La muhimu ni kwamba mbali na hayo, itashawishi wanafunzi kuchangia darasani na kubadilisha mawazo wakifunzana wenyewe kwa wenyewe. Mkakati huu ina wepesi wa kutekelezwa na haitoingilia masomo mengine wala kazi wanafunzi na walimu wanazowajibika kutekeleza katika mfumo wa 8-4-4.
Harakati hizi zitahusisha usaidizi kutoka kwa Walimu Wakuu. Katika mashule yao, wakuu hawa watawajibika kutenga siku moja kwa wiki kama Jumatano kwa mfano. Siku hii itatumika kama siku rasmi ya Kiswahili kwa walimu, wanafunzi na waliojiriwa na shule. Mawasiliano nje ya darasani itatekelezwa kwa Kiswahili. Kuanzia matangazo ya gwaride la asubuhi, maombi kabla ya mamkuli, mazungumzo ya kibinafsi katika Jumba la mamkuli na hata mazungumzo katika zahanati na mwuguzi wa shule. Yapasa kutekeleza mpango huu bila ya utumizi wa mabavu kwani itaashiria adhabu kwa wanafunzi na watakaidi amri. Mfumo wa 8-4-4 hausisitizi masomo nje ya darasa kupitia mazungumzo, michezo na mambo ya kawaida tunayotekeleza kila siku. Ni vigumu kueleza umuhimu wa masomo nje ya darasa, hasa kwa wale miongoni mwetu tuliopitia 8-4-4. Mpango huu ukifuatiliwa na mashule za kuanzia utotoni, utasisimua ubongo wa mwanafunzi kujua kwamba Jumatano ni siku ya Kiswahili. Mtindo huu ukiendelezwa kila wiki katika maisha ya mwanafunzi, itazidi kuimarisha ufasaha wake na kuongezea makali kwa ubongo wake katika kuelewa lugha ya Kiswahili. Tukumbuke kwamba hatua hizi haizidishi uzito wa wajibu wa masomo mengine. Badala ya kusimua na kuchambua visa vya Mwalimu Jini, wanafunzi wataanza kuchipua mazungumzo kuhusu mambo ya kijamii, Michezo na mambo mengine mengi inayowahusu. Mazungumzo na mijadala hii ya hali ya juu ndizo zitakazong’olea nanga lugha ya Kiswahili na kuzidi kusambaza umaarufu wake.
Hatua ya tatu, ni kushurutishwa kwa mashule ya msingi na wizara ya elimu kufunza somo moja kikamilifu kwa lugha ya Kiswahili. Hatua hii itazua changa moto kwani itahitaji mamlaka ya kiserikali. Wazo la baadhi ya wana-chuoni wa Kiswahili ni kufuata mwongozo wa Tanzania na kufunza masomo yote kwa Kiswahili. Wazo hili japo si baya, litazua ugumu wa utekelezaji kwa ajili ya ukosefu wa miundo-mbinu mwafaka nchini Kenya na vile vile si jambo linalohitajika. Watanzania wana miundo-mbinu kabambe na uwezo wa kutekeleza Mafunzo ya kimsingi kwa Kiswahili, lakini mfumo wao wa elimu una changa-moto zaidi ambazo tutakabili baadaye. Nchini Kenya, kuna uhaba wa walimu na wataalamu wa Kiswahili na kufasiri masomo yote kwa Lugha ya Kiswahili ni Jambo litakoluwa na ugumu wa hali ya juu kutekeleza. Zaidi ya hayo, Lugha ya Kiswahili na Kimombo zaweza kustawi pamoja kwa njia mwafaka itakayotuwezesha kuimarisha umahiri katika Lugha zote mbili. Tutajadili swala hilo katika nakala litakalofuata. Somo ambalo ningelipendekeza ni somo la ‘Maadili ya Kijamii’ (Social Ethics) linalofunzwa kwa Kiingereza kufikia sasa. Masomo mengine ya msingi ni Hisabu, Sayansi na GHC lakini kupendekezwa kwa somo la ‘Maadili ya Kijamii’ ni kwasababu ya wepesi na urahisi wake wa kutekelezwa. Masomo mengine yenye uzito itazua matatizo kufasiri na kuwaelimisha walimu kuwawezesha kufunza masomo haya kwa Kiswahili. Zaidi ya hayo, uhaba wa wakati, utaalamu na nia kutoka washirika dau wa elimu itazua matatizo zaidi.
Pendekezo kuu ni kufasiri vitabu na masomo yote ya ‘Maadili ya Kijamii’ kwa lugha Kiswahili, kisha kutoa mafunzo kwa Walimu wa Kiswahili kuwawezesha kutekeleza mafunzo ya somo hili kwa Kiswahili. Hatua hii itasambaza ajira kwa walimu wa Kiswahili na kuchipua mwamko mpya kati ya walimu wa Kiswahili. Zaidi ya hayo, itawapa wanafunzi fursa ya kuweza kujitosa na kuogelea katika bahari la Kiswahili. Katika mafunzo ya lugha, kuna wajibu wa kujitosa kikamilifu. Kujitosa hutofautisha ujuzi kama mfano ya mchezaji ambaye hufanya mazoezi tu mara kwa mara na yule ambaye amepata fursa ya kucheza katika mechi kadhaa. Inaweza kulinganishwa pia na mwogeleaji ambaye huoga katika kijidimbwi kidogo na wale ambao hupiga mbizi na kuoga katika Ziwa, Mto au Bahari yenye mawimbi. Mafunzo ya Kiswahili kama somo la kando itatuwacha tukiwa wachezaji wa mazoezi na waogeleaji wa vijidimbwi. Kawaida yetu Wakenya, tukikabiliwa na maswala muhimu kwa Kiswahili, aidha tutazama au kukaukiwa na mawazo. Wakenya wana ufasaha wa hali ya juu katika uandishi, mazungumzo na usomi kwa lugha ya Kiingereza. Chanzo cha umahiri huu ni kule kujitosa vikamilifu katika masomo ya Hisabu, Biolojia, Historian a kadhalika kwa lugha ya Kiingereza. Mawazo katika Kiingereza hututiririka bila ya kusita ilhali Kiswahili chetu kinakumbwa na upungufu wa mawazo. Mfumo wa elimu ukishurutisha wanafunzi kujitosa katika somo moja kwa lugha ya Kiswahili, itaimarisha viwango vya utumizi wa lugha maradufu bila ya kuikandamiza masomo ya Kiingereza. Mawazo yataanza kutiririka kwa urahisi. Wenzetu Watanzania wanakumbwa na changa-moto sawia kwa lugha ya Kiingereza. Wanahitaji kutekeleza mbinu sawia na Kenya kwa kinyume. Hivi ni kumaanisha, washurutishe somo moja la kufunzwa kwa Kiingereza katika shule ya msingi. Vile vile, wawasilishe siku Fulani iwe siku rasmi ya kuzungumza Kiingereza, na walimu wa Kiingereza walete ubinifu wao katika kujadili mada darasani. Katika nchi zote mbili, hatutazamii kufuruga au kuvunjilia mbali mbinu zilizomo kwa sasa. Ni mambo na kuleta mabadiliko chache ili kustawisha miundo-mbinu iliyomo kufikia sasa na vile vile kurekebisha na kukarabati upungufu uliomo. Katika mipango ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ya kutaka kuleta Uhuru wa Kazi kupitia mipaka, inapasa tuwashawishi walimu Watanzania wa Kiswahili kuvuka Kenya na Walimu Wakenya wa kiingereza kuvuka Tanzania kutuwezesha kuimarisha lugha zote mbili.
Mikakati hii tuliyoangazia kufikia sasa ni hatua za kwanza muhimu zitakazoleta matokeo ya kuridhisha miaka ya karibuni. Hatuna uwezo wa kutoa thibitisho ni kiwango gani itatufikisha lakini matokeo ya mitihani ya Kiswahili ya Kitaifa itaanza kuimarika . Viwango vya uandishi wa Insha na uandishi wa kitaalamu pia vitaimarika. Mfumo wa elimu wa Kenya, itawajibika kupanga mikakati ya kuwawezesha wanafunzi wanaorejea kutoka ng’ambo kuweza kujiimarisha katika lugha ili kufikia viwango vya wenzao. Mipango itakuwa msaa mkubwa pia kwa wanafunzi wahamiaji au wakimbizi waliotoweka vita na vurugu katika nchi zao. Kuna umuhimu wa kurahisisha somo la Kiswahili kwa yeyote aliye mtaalamu na hata kwa wanaoanza kujifunza lugha hii. Itatuwezesha kumaliza ule mtazamo unaoangazia Kiswahili kama somo ambalo ni kizuizi kwa matokeo bora katika mitihani. Wana-chuoni kama Ahmed Nabhany wamependekeza lafdhi nyingine mbali na ile ya ‘Kiunguja’ zifunzwe shuleni. Wazo lenyewe si baya lakini wana-chuoni wanapasa kuelewa kwamba watu wanatofautiana katika wepesi wa matamuzi ya Lugha. Tusiporahisisha mbinu za mafunzo ya Lugha hii yetu, tutaanza kupoteza mwongozo na mwelekeo wa lugha. Kinyume na wana-chuoni, kuna baadhi ya watu walionda umbali wa kupendekeza somo la Kiswahili lifutiliwe mbali kutoka mfumo wetu wa elimu. Kwa maoni yangu, hii ndiyo itakuwa mizizi ya kutofaulu kitaifa hasaa tukizingatia ukabila unaotukumba. Duru za utafiti zinaonyesha kwamba kuelewa zaidi ya lugha moja , inatuwezesha kujizatiti vilivyo katika lugha nyingine na huzipa ubongo makali zaidi. Kwa vyovote vile kuimairisha lugha itamfaidi kila mtu.
Tukiweza kufaulu kuyakusanya na kujumuisha mawazo haya, Wizara ya elimu itawajibika kuieneza mafunzo ya Kiswahili katika vyuo vikuu na kuongeza ufadhili kwa mafunzo yaliyomo kufikia sasa. Zaidi ya hayo, watawajibika pia kuwapa vijisababu wanafunzi waliotoa matokeo bora katika mitihani kutaka kuendeleza masomo yao ya Kiswahili. Vijasababu kwa mfano ni kupunguziwa ada ya karo, Uthibitisho ya kutunukiwa kazi wakiwa chuoni, malazi bora zaidi katika vyuo na kadhalika. Vijisababu vya kusoma Kiswahili vikiimarishwa, vyuo vyetu vitajumuisha vipaji bora zaidi nchini na kuanzisha mwamko mpya wa wasomi wa Kiswahili wa Kizazi Kipya ambao ni vijana mabarobaro wanaoambatana na miondoko ya enzi ya kisasa. Mipango hii itazua ajira mpya kwa Wakalimani wa hali ya juu, wahauri wa masomo ya Kiswahili na hata maprofesa watakaofunza Kiswahili katika vyuo vya nchi mbali mbali. Mipango hii inatazamia kukuza lugha ya Kiswahili na kuiwezesha kuimarika katika karne ya ishirini na moja na vile vile kuongeza ajira zinazohitajika kwa dharura nchini Kenya.
Katika jukumu letu kama wamiliki wakuu wa Lugha, Kenya yahitaji Taasisi maalum ya Kiswahili. Tutaifananisha taasisi hii na Alliance Française ya Wafaransa. Taasisi hii itatoa mafunzo ya kuanzia makurutu hadi wataalamu wa Kiswahili toka nchi za kigeni na Wakenya waliozaliwa na kuishi Ng’ambo. Tutayaazima mawazo kutoka ‘Taasisi ya Lugha’ toka kisiwa la Unguja ambapo masomo ya Kiswahili haikomi darasani. Wanafunzi wataishi na jamii za karibu ili kuwawezesha kufanya mazoezi ya mazungumzo kila kukicha. Wanafunzi watahusishwa katika mambo ya kawaida kama kwenda Sokoni, Uvuvi, kuhudhuria maharusi na watasaidia pia katika kazi za kinyumbani. Masomo yatajumuishwa kwa ya miezi mitatu, miezi sita miezi tisa au mwaka mmoja. Mipango pia ya kujumuisha masomo ya wiki kadhaa au mwezi mmoja hasaa kwa Watalii itaundwa, na kutuwezesha kuanza sekta mpya ya ‘Utalii wa Lugha.’ Haya ni mapendekezo makubwa mno lakini chini ya uongozi angalifu na Wizara ya Utamaduni na Turathi za kitaifa, yote yatawezekana. Kufikia sasa, sijaelewa ni mipango gani iliomo katika Wizara hii katika kuhifadhi tamaduni na turathi zetu. Mawazo ya Wizara ya Utalii itahusishwa baada ya Taasisi kuanza kutoa mafunzo. Tungependekeza sehemu ya kwanza aidha kuwa Mombasa, Kilifi au Malindi kwasababu ya kuwemo na wasemaji wa Kiswahili maridhawa na huduma zinazohitajika na Wageni nchini Kenya. Kenya itakapoanza kukaribia viwango vya Kiswahili vya Tanzania, tutaweza kuongeza taasisi hizi kwa mikoa nyingine ili kuweza kukidhi mahitaji ya Kiswahili maradufu. Isitoshe, Taasisi hii itakuwa chanzo cha ajira kwa Wataalamu wa Lugha, Washauri na hata Wafuta Madirisha. Zaida ya hayo, vitakuwa vituo vya Utamaduni ambapo kongomano zitaandaliwa kuangazia mambo ya Kitamaduni, Kijamii na Kiuchumi kwa lugha ya Kiswahili. Tukishafaulu nchini Kenya, Serikali yetu ikishirikiana na Mabolozi yake Ng’ambo, itawajibika kueneza wazo hili kwa nchi geni kama Wafaransa walivyotoa mwongozo na Kifaransa. Kama kianzilishi, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini zingepewa kipo umbele katika hali ya kudumisha Muungano wa Afrika ya Mashariki. Zaidi ya hayo, mabalozi yetu yataendelea kuinadi lugha iwe lugha kuu ya Afrika Mashariki na hata Afrika kwa ujumla. Tukijikakamua na kufanya kazi kwa bidii, yote yatawezekana.
Falsafa za Google zimechacha hii leo na tumshukuru Mola kwani sisi si maprofesa wa Mtandao. Kama Wakenya tushukuru kwa Baraka tulioyotunikiwa ya kuwa na Lugha ya Kitaifa. Rafiki Mzungu wa umaarufu wa ‘Kipande cha Keki,’ alinitajia mambo ambayo kwa ujumla Wakenya na Wafrika hupuuza. Alinieleza kwamba Wafrika wa Magharibi walihifadhi mavazi lakini wakapoteza lugha zao kwa Kifaransa. Wafrika wa Mashariki nao walipoteza mavazi kwa minajali ya mavazi ya Kizungu lakini walihifadhi lugha zao. Aliendelea kwa kunieleza Kenya na Tanzania ndizo nchi za kipekee za kiafrika (za makabila kadhaa) zilizo na lugha ya kitaifa ya kiafrika. Maneno makali sana toka kwa mzungu kuhusu Afrika. Nchini Kenya, tuliandaa katiba mpya ya hali ya juu hivi basi kuitunuku Kenya kuwa nchi la pekee lililo na Katiba lililobuniwa Afrika, kuandikwa na Wafrika kwa manufaa ya Wafrika. Jukumu imetuangukia sisi wenyewe kuyaleta mabadiliko au kutazama tu mambo yakibadilika mbele zetu. Azimio langu ni kubadilishana mawazo ili tupate ufahamu zaidi kwani hakuna aliye na mawazo yote mazuri. Ninatazamia kupata fursa ya kukutana na maafisa wa Elimu tuweze kuyajadili mawazo haya kwa undani. Haya ni mawazo kamili wala si ya kubuni, zinazotokana na uhusiano wangu na wakenya dunia nzima. Katika nakala yangu ifuatayo, tutaangazia Lugha za Kitamaduni nchini Kenya. Hatutoanza kuyajadili kwa sasa lakini ningependa kukusanya mawazo ili tuweze kupata nakala nzuri. Kijana wenu Mteule Yule Yule, anawaaga na kuwatakia wiki njema.
No comments:
Post a Comment