Falsafa za Google na Maprofesa wa mtandao wamezonga mtandao wa internet na ulimwengu tangu mtandao ilipoenezwa kwa Jumuiya. Wana-Falsafa wa Google na Maprofesa wa mtandao kwa ufupi, ni watu walio na dhana kwamba wanajua mengi na kujidai kuwa wana-chuoni katika mada mbali mbali, Kisababu ikiwa wanamiliki mitambo ya tarakilishi na uwezo wa kuifikia tovuti ya Google.com. Kwa upande wa Google, ni chombo muhimu ikitumika inavyostahiki kwa minajili ya usaidizi. Yaweza kuwa hatari mno ikitumika kama nyongeza ya ubongo na hukandamiza uwezo wako kimafikra. Kwa upande mwingine, kwa kila Mwana-Falsafa wa Google na Profesa wa Mtandao kati yetu, kuna wale ambao wanakiri kutojua na wana ari ya kutaka kufahamu. Muhimu zaidi, kuna watu waliojitolea kwa hali na mali katika mada tofauti na kuhitimu kama wana-chuoni katika mada hizi. La kusikitisha zaidi, ni hawa Maprofesa wa mtandao ndio wanaopaza sauti na kujigamba zaidi, na Blogu hii imetungwa kwa niaba yao kuwarudisha ughaibuni.
Kwa nakala hili la kwanza, tutaanza kwa utaratibu bila ya mpangilio maalum. Lengo kuu ni kupata fursa ya kuyajadili maoni na mawazo tofauti kulingana na malezi yetu ya kipekee na matukio kimaisha kwa ujumla. Tutaangazia Michezo, Siasa, Teknolojia, Uhusiano wa kimataifa, Mambo Yaliyomo, Maswala ya Kijamii, Historia, Sanaa, Utamaduni, Lugha na Uandishi wa Habari. Hakuna mada yoyote maalum itakayotuzwa kipo umbele. Nakala itachapishwa kulingana na matukio miongoni mwetu za hivi karibuni. Nakala hizi zitamulika mitazamo tofauti kulingana na hali ya maisha katika mitaa ya Kenya na maisha nchini Marikani kwa wahamiaji wenye asili ya Kiafrika. Uandishi huu utaelekezwa na mwongozo wa kuwemo kadmanasi ya malimwengu mawili yaliyotofautiana na vile vile kukurubiana! Tumejitenga katika sehemu hii kwani mitandao kama ya 'Facebook' na 'Twitter' si vikao mwafaka vya kubadilishana mawazo kwasababu ya sehemu dogo iliyomo na msongamano kwa ujumla. Katika tovuti za 'Facebook' na 'Twitter,' kuna kujidai kwingi, kutayarisha maoni na kujipaka mafuta katika hali ya kujisifu. Ni nadra sana kupata ukweli katika tovuti hizi lakini kuna 'wasomi' wengi wa mtandao wanaohubiri falsafa zao za tovuti ya 'Google.'
Jambo la kipekee cha kutofautisha blogu hii ni kuwa nakala zitachapishwa kwa Kiingereza na kufuatiliwa punde na tafsiri ya neno kwa neno au wazo kwa wazo kwa lugha ya Kiswahili. Moja kati ya sababu za kufanya hivi ni kuwa hakuna nakala za kutosha katika mtandao kuwapa mazoezi wanafunzi wa Kiswahili wasio na asili ya Afrika Mashariki. Kasoro tovuti kadhaa za Kitanzania na kanda chache za 'Youtube', Wazungumzaji wa Kiswahili na wanafunzi wa Lugha vile vile hawana jukwaa katika mihadhara ya mtandao wanapoweza kujumuika na kukabiliana na maswala nyeti. Cha kusikitisha zaidi, ni kwamba hakuna Radio au Runinga katika mtandao inayopeperusha vipindi vyake moja kwa moja kwa lugha ya Kiswahili! Hii ni aibu kubwa sana ukizingatia kwamba vipindi vya Radio vinapeperushwa moja kwa moja kwa Lugha za Kishona (Zim Net Radio), Kikalenjin (Kass FM) na Kikuyu (Kameme FM). Nawapongeza Wakurugenzi wa radio hizi kwa kuwafikia na kuwapatanisha wasikilizaji wao moja kwa moja katika mtandao. Kwa wanaotumia simu za iPhone na Android, kuna 'Kijiprogramu' kinachokufikishia radio mbali mbali duniani katika mtambo wako kulingana na nchi, jiji, Lugha na njia nyingine mbali mbali za kutafuta. Katika sehemu iliyotengewa Kenya na Tanzania, aidha stesheni za radio hazimo au zilizomo hazifanyi kazi? Tutawaibisha kidogo 'Radio Maisha' nchini Kenya iliyo katika miliki ya 'Standard Media Group,' kisababu ikiwa wana Magwiji waliobobea katika lugha ya Kiswahili na wana vipindi vya kusisimua mno na bado masafa yao haipatikani katika mtandao kufikia hadi sasa. Matumaini ni kwamba moja wao ataisoma nakala hii na kuwaarifu wakurugenzi kuhusu swala hili. Hatutosita pia kuwakemea 'Nation Media Group,' 'Kenya Brodcasting Corporation (KBC)' na nyingi kati ya Radio za Tanzania zinazosambaza matangazo na vipindi kwa Kiswahili.
Katika miaka ya hivi karibuni, Sanaa imejitokeza zaidi na kuyachemsha mawazo yetu. Ubunifu wa Kisanii ni jambo la usiri lakini matokeo hutuacha kwa butwaa. Tukimnukulu mwana-harakati mashuhuri wa mageuzi nchini Kenya Mchungaji Timothy Njoya katika mahojiano na Mwandishi wa Habari wa K24 Jeff Koinange, "Unda mabendi na wakusanye vijana wanaohudhuria hii mikutano ya kisiasa kisha uwalipe wakishatunga ngoma na nyimbo za kusisimua...tuwahimize vijana wetu kuwa wasanii kwani wana vipaji..." Wengi wetu tuliozaliwa na kulelewa barani Afrika katika kizazi hichi kipya, hatukupata fursa maalum ya kujitosa katika Ulimwengu wa Sanaa hapo awali lakini 'Simba mwenda Pole ndiye Mla Nyama.' Kwa vyovyote, Afrika ndo chanzo na kiini cha Sanaa. Hakuna aliyewafunza Wakisii nchini Kenya kuyachonga mawe ou WaGaa kutoka Ghana kuyatengeza Majeneza ya kustaajabisha na WaFulani wa Senegal Kucheza densi kama nyoka na kupigisha miguu kama Jeshi. Falsafa za 'Google' zimetosha kwa sasa lakini kuna umuhimu wa kuwasaka Maprofesa wa mtandao. Watu hawa ni mfano wa Kirusi kisichojulikana na linalozidi kuenea. Tunatarajia na tutafurahia maoni yoyote ya kutuwezesha kuimarisha maandishi na nakala zetu. Tutajaribu tuwezavyo kuchapisha nakala kila Ijumaa. ikumbuke siku ya Ijumaa kwa kutia alama kwa kalenda. Ni mimi Kijana wenu yule yele Mteule akitamatisha na kuwatakia wiki njema.
No comments:
Post a Comment